MGOMBEA uraia wa Jamhuri ya Muungano kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Magufuli, jana amewasili Zanzibar na kupata mapokezi makubwa akiongozana na mgombea mwenza, Bi. Samia Suluhu Hassan na kuwaahidi Wazanzibari kuwa hatowaangusha.
Viongozi hao wapo Zanzibar kwa ajili ya kutambulishwa sambamba na kutoa shukurani zao kwa kuungwa mkono na wana CCM.
Mwenyeji wao Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein, aliwatambulisha rasmi viongozi hao kwa wana CCM na wananchi waliofika katika Viwanja vya Ofisi ya CCM Kisiwandui Mjini Zanzibar.
Dkt. Magufuli aliwahutubia wana CCM na wananchi waliohudhuria katika mapokezi hayo ambapo kabla ya utambulisho alizuru kaburi la Muwasisi wa Mapinduzi, hayari Mzee Abeid Amani Karume na kumuombea dua.
Katika hotuba yake, alitoa ahadi kwa wana CCM na wananchi akisema hatawangusha na kuwahakikishia ushirikiano ili Tanzania izidi kupata maendeleo ya kutosha.
Alisema katika mchakato wa kumtafuta mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano, kulikuwa na makundi 42 ndani ya CCM lakini hivi sasa limebaki moja tu akiwataka wanachama kushikamana ili chama hicho kiweze kupata ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Aliahidi kuitekeleza Ilani ya CCM wakati utakapofika hasa kwa kuzingatia mambo mbalimbali yaliyoelezwa kwenye ilani yakiwemo, biashara, kilimo, uvuvi, ujezi, barabara gesi na mengineyo.
Alisema yeye, Rais Dkt. Shein na Bi. Hassan wataendelea kuitetea CCM, kuutetea Mungano na maendeleo ya Watanzania wote. Pia alimsifu Dkt. Shein akisema ni kiongozi mwenye huruma, anayependa wananchi wake, asiye na majivuno na mpenda maendeleoa.
Nae Bi. Hassan alitumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa mapokezi hayo na kuwashukuru viongozi kwa kujali nafasi za wanawake ambao aliwataka waipigie kura CCM katika uchaguzi ujao.
Dkt. Shein alimpongeza Dkt. Magufuli na Bi. Hassan wana uwezo mkubwa wa kuongoza nchi, kuujua Muungano na Mapinduzi ambapo kupata nafasi hizo ni haki zao.
No comments:
Post a Comment