
ZAIDI ya dakika 57, zilitosha kumtoa ‘jasho jembamba’ msanii mwenye nyonga laini na kiuno bila mifupa, Rehema Chalamila ‘Ray C’ kuhaha ili afanikiwe kumfikia kwa ukaribu Rais Jakaya Kikwete‘Katukio hako ka’kiaina’ yake kalijiri Alhamisi iliyopita ndani ya Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar, kulikokuwa na hafla maalum iliyoandaliwa na umoja wa wasanii kwa ajili ya kumuaga Rais Kikwete.
Awali, kabla ya Rais Kikwete kuingia ukumbini humo, mwandishi wetu alimshuhudia Ray C akiwa amekaa kwa staili ya ‘kusikiliza misa’ akiwa sanjari na wasanii wenzake akiwemo ‘pacha’ wake, Winfrida Joseph ‘Recho’.
Hata hivyo, mambo yaligeuka baada ya rais kuingia, ambapo paparazi wetu alimuona Ray C akihangaika kwa kuhama sehemu moja kwenda nyingine, akitafuta upenyo wa kukaa karibu na rais lakini mfumo wa ulinzi uliokuwepo, ulimzuia kutimiza azma yake hiyo.
Baada ya kuona Ray C akiwa hana amani, mwandishi wetu alimfuata na kumuuliza kulikoni alionekana kuhaha ukumbi mzima, ndipo alikiri kuwa alikuwa akihangaika kutaka kukaa karibu na Rais Kikwete.

“Yaani we acha tu, nahangaika angalau niweze kumsalimia baba yangu huyu, nadhani unajua fika jinsi alivyonisaidia, sasa akiondoka ukumbini humu bila angalau kumsalimia, nitajisikia vibaya sana, lakini naona kuna ugumu kutokana na walinzi kumbana sana, sijui hata nifanyaje,” alisema Ray C huku akionesha uso wa hamaki.
Hata hivyo, jitihada za msanii huyo kukutana na Kikwete zilizaa matunda wakati wa kucheza muziki ambapo rais aliyekuwa akilisakata dansi vilivyo katika ‘dance floor’, alikutana naye, wakasalimiana na kucheza pamoja.
No comments:
Post a Comment